Sote tunafahamu kwamba elimu Tanzania iko katika hali ya mbaya. Viwango vya ufaulu vimeporomoka kwa wengi. Hakuna vitabu vya kutosha. Ufundishaji duni. Na matatizo mengine mengi.

Sasa utafanya nini kama wewe ni mzazi, kaka au dada na unataka kutafuta shule bora? Inakuwaje kama wewe ni diwani au kiongozi mkubwa wa Serikali na unataka kufuatilia maendeleo? Kwa sasa ni vigumu mno kufanikisha hayo, kwa sababu taarifa hizi hazipatikani kirahisi. Na pale zinapopatikana, ni ngumu kuzielewa na hata kuzitumia.

Je, data zilizo wazi zina maana gani kwa kila mmoja wetu? Je, hii ni dhana tu iliyo kwenye vichwa vya marais na wabunge? Au ina matumizi zaidi? Data zilizo wazi kwa kweli zina maana kwetu sote katika kutoa uamuzi ulio sahihi. Kama mtu akifahamu ni dawa zipi zinapatikana katika kituo cha afya kilicho karibu, basi tungeokoa muda kwa safari zisizo na tija. Kama tungekuwa tunapata taarifa kuhusu hali ya barabara basi tungepangilia vema zaidi safari zetu. Na kama tungekuwa na taarifa kuhusu viwango vya ufaulu vya shule, basi tungekuwa na fursa ya kufanya uchaguzi bora zaidi kuhusu elimu ya watoto wetu na hivyo kuzuia uwezekano wa wao kufeli hapo baadaye.

Sisi, kama vijana wa kitanzania, tuliona kwamba hakukuwa na hata chanzo kimoja cha data za mitihani ya kitaifa katika nchi yetu. Zile zilizopo, zimekaa kwenye makabrasha ya ripoti na nyingine kutawanyika kwenye mtandao huku na kule. Tuliamua kukusanya data hizi ili zipatikane kwa urahisi zaidi. Tulivutiwa zaidi na data za kitaifa, kimkoa, kishule na za mtahiniwa mmoja mmoja ili tuweze kuwasilisha taarifa zenye kufaa zaidi kwa kila mmoja anayejali kuhusu elimu, kuanzia wazazi hadi watunga sera.

Kwa miaka miwili tumekuwa tukiandika namba maalumu inayonyumbulisha data za elimu kutoka katika vyanzo tofauti katika mtandao wa Intaneti. Tulithibitisha data, tulizikusanya na kuziweka katika namna inayonyumbulika zaidi ili watumiaji waweze kuzitumia, na kuchota taarifa zile wanazoona zinawafaa zaidi wao.

Tulipokuwa katika mchakato huu, matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne ya 2012 yalitangazwa. Tulifikiri kwamba hiyo ilikuwa fursa kwetu kuweka mkazo zaidi na kumalizia kazi yetu iliyokuwa ikiendana sana na suala hilo. Kwa hiyo, tumeandaa tovuti hii ambayo inawasilisha data za matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne kurudi nyuma hadi mwaka 2004* kwa ngazi za mtahiniwa, shule, somo, mkoa na kitaifa.

Tunapotazama mbele, tunakusudia kuingiza pia matokeo ya vidato vya 2 na 6. Tunatumaini kuwa tovuti hii na data zilizomo zitakuwa chanzo muhimu cha taarifa na kutuelekeza wote katika majadiliano yenye nguvu za hoja kuhusu sekta yetu ya elimu. Tunatumaini wazazi wataweza kutumia data za shule ili kuchagua shule za kumpeleka mwanao huku wakiwa na ushahidi wa takwimu shule hizi. Tuna matumaini kwamba watunga sera watatumia hii kuchunguza mienendo na mielekeo ya kila mwaka ili kufanya mabadiliko yanayohitajika katika sera ya elimu na utekelezaji wake. Tungependa wenzetu katika vyombo vya habari kutumia data hizi kutoa taarifa na kuandika habari za masuala ya elimu. Na tunatoa huduma ya kadi za ripoti kwa ajili ya wanafunzi ili kwamba waweze kupata kwa urahisi na mara moja matokeo yao.

Tunakaribisha maoni,mapendekezo na ukosoaji ili kuhakikisha kwamba tovuti hii inakuwa kitu kilicho hai na kinachoweza kuwa rasilimali muhimu. Pia tunakaribisha uchambuzi zaidi na matumizi ya data na tungewahimiza muwasiliane nasi kama unaweza kutengeneza visaidizi vya kuonyesha data vya nyongeza na uchambuzi.

Tutaendelea kuongeza ubora na kuweka taarifa mpya kadiri data zinavyozidi kupatikana. Data zote kuhusu visaidizi vya kuwezesha data kuonekana katika wavuti hii vinaweza kupakuliwa. Katika majuma yajayo, tutafanya visaidizi hivi ya data kuonekana ili viweze kunakiliwa kwa urahisi zaidi.

Takwimu zilizowekwa kwenye wavuti hii ni sahihi, kadiri ya uelewa wetu, lakini usahihi huo hauwezi kuhakikishwa kwa sababu tumenakili kutoka katika vyanzo mbalimbali. Vyanzo vya data

Kazi ya Tovuti imefanikiwa kutokana na ushirikiano na Twaweza

Ujumbe kutoka kwa Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza

Kulingana na kanuni za mpango wa kimataifa wa kuendesha shughuli za Serikali kwa uwazi (OGP) na haki ya kupata taarifa, Twaweza inaamini katika thamani ya taarifa na data kuwa wazi kwa umma. Pale taarifa inapopatikana, watu wanakuwa na ufahamu, mijadala ya umma inakuwa imejaa taarifa, hii inakuza ushiriki na kuleta maamuzi mathubuti. Hii ndiyo maana Twaweza inafurahia na kuunga mkono juhudi za vijana wa kitanzania kufanya data za elimu, zilizokusanywa toka tovuti mbalimbali, kwamba watu wazipate kwa urahisi. Tunawahimiza, watembeleaji wa tovuti hii, waitumie kupata uelewa wa elimu ya Tanzania, na watumie taarifa hizo kuchukua hatua. Tovuti hii, ni mwanzo tu, sio kamilifu. Hivyo, tunawakaribisha wote kutuma masahihisho na maoni kwa timu inayoratibu Shule.info, ili kuboresha tovuti hii kwa manufaa ya wote.

Vyanzo

2004 http://www.tanzania.go.tz/matokeo2004/OLEV2004.HTM
2005 http://www.tanzania.go.tz/NectaResults2005/OLEVEL.htm
2006 *
2007 http://www.tanedu.org/csee2007/olevel.htm
2008 http://www.matokeo.necta.go.tz/olevel2008.htm
2009 http://www.matokeo.necta.go.tz/matokeo_html/csee2009/olevel.htm
2010 http://www.matokeo.necta.go.tz/matokeo2010/csee2010/olevel.htm
2011 http://www.necta.go.tz/2011/matokeo/csee2011/olevel.htm
2012 http://www.necta.go.tz/matokeo2012/csee2012/olevel.htm

*Tafadhali zingatia kuwa takwimu za mwaka 2006 hazikuingizwa katika wavuti hii ikiwa ni kwasababu hazikupatikana katika mtandao wowote wenye takwimu zilizochapishwa na NECTA.

*Tafadhali zingatia pia kwamba kuna uwezekano baadhi ya vyanzo au vyanzo vyote hapo juu havifikiki tena.

Matokeo yalifanyiwa kazi vipi?

Programu maalumu za kompyuta zilitumika kuchuja matokeo yaliyochapishwa na NECTA, na hizi zilisaidia kupatikana kwa seti za takwimu zilizo kwenye wavuti hii.

Kutengeneza matokeo nyumbulishi ya shule na mikoa yanayotumika kulinganisha shule na mikoa, uamuzi na nadharia zifuatazo zilitumika:

  • Ni matokeo halali ya watahiniwa waliopata kati ya pointi 7 na 35 tu ndiyo yaliyotumika. Mengine yaliachwa. Watahiniwa walioachwa ilihusisha wale waliosajiliwa lakini ambao hawakuwepo na wale ambao walipewa matokeo mengine na NECTA ukiacha ya daraja la I, II, III, IV na waliofeli.
  • Wastani wa pointi zilizotumika kulinganisha mikoa na shule ni wastani wa pointi mnyumbuliko kwa watahiniwa wote waliopata matokeo halali katika mkoa au shule kama yalivyochapishwa na NECTA.